Aisha Masaka aweka historia kucheza UEFA

KANDANDA Aisha Masaka aweka historia kucheza UEFA

Na Zahoro Mlanzi • 21:45 - 16.11.2023

Nyota huyo ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars', amejiunga na BK Hacken akitokea Yanga Princess

Mshambuliaji wa Kitanzania, Aisha Masaka, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kwa upande wa wanawake kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya Jumanne usiku kuisaidia timu yake ya BK Hacken kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Paris FC.

Nyota huyo ambaye ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars', ameanza katika mchezo huo ambapo mabao ya ushindi kwa timu yake yalifungwa na Anna Sandberg na Rosa Kafaji.

Masaka alijiunga na miamba hiyo ya Sweden, msimu uliopita akitokea kwenye Klabu yake ya Yanga Princess.

Tangu amejiunga na timu hiyo amekuwa katika kiwango kizuri huku akiisadia timu yake kushinda michezo mbalimbali na yeye akiwa sehemu ya kikosi.

Baada ya mchezo huo, Hacken sasa inaongoza Kundi D ikiwa na alama 3 huku timu za Chelsea na Real Madrid zikifuata baada ya kutoka sare ya 1-1 kwenye mchezo wao na Paris wakiburuza mkia wakiwa hawana alama.

Timu zote zimecheza mchezo mmoja na katika mechi ya pili Hacken wanatarajia kuwa nyumbani kuwaalika Real Madrid.

Tags: