Azam FC yatamba kutoa dozi zaidi

LIGI KUU Azam FC yatamba kutoa dozi zaidi

Na Zahoro Mlanzi • 19:00 - 10.12.2023

Timu hiyo kwa sasa ndio inaongoza Ligi Kuu Tanzania ikiwa na alama 25 ikifuatiwa na Yanga yenye alama 24

Vinara wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, timu ya Azam FC, imetamba kuendeleza ubabe wao kesho wakati watakaposhuka kwenye uwanja wao wa Chamazi Complex kucheza dhidi ya JKT Tanzania.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa saa 1 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Azam imekuwa katika kiwango bora kwa mechi za hivi karibuni wakiwa na jumla ya mabao 15 katika mechi zao nne za mwisho walizocheza.

Katika mchezo wa mwisho waliocheza wiki iliyopita waliwafunga KMC kwa mabao 5-0 kama walivyofanya kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Akizungumza na Pulsesports, Meneja wa Habari wa timu hiyo, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi', amesema wanatarajia kundeleza dozi hizo kwa timu zote ambazo bado hawajacheza nazo kuelekea kumaliza duru ya kwanza ya ligi.

"Kwasasa tupo katika kiwango kizuri na tunatarajia kuendelea kufanya vizuri ili kujiweka katika nafasi ya kugombea nafasi za juu mwisho wa msimu," amesema.

Azam kwa sasa inajivunia pia kiwango bora cha Kiungo wao wa kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye hadi sasa anaongoza kwa upachikaji mabao akiwa amemtupia 7 sawa ma Jean Baleke wa Simba na Max Nzengeli wa Yanga.

Hata hivyo, Azam ipo mbele kwa michezo miwili zaidi ya Yanga na Simba ambazo zilikuwa katika majukumu ya mechi za kimataifa.

JKT Tanzania wao wana alama 16 wakiwa nafasi ya nane. Wanaingia katika mchezo huo wankesho wakiwa na kumbukumbu ya sare ya 2-2 dhidi ya Singida FG.

Tags: