Michuano hiyo itafanyikia visiwani Zanzibar kuanzia Desemba 28 huku ikipangwa katika makundi matatu tofauti
Timu ya Bandari FC, imepangwa Kundi C pamoja Yanga SC katika michuano ya Mapinduzi Cup itakayofanyika visiwani Zanzibar kuanzia Desemba 28.
Mbali na timu hizo, pia Vital'O ya Burundi na KVZ zinaungana na miamba hiyo katika kundi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Mashindano hayo, mabingwa watetezi wa kombe hilo, timu ya Mlandege FC, imepangwa Kundi A pamoja na Azam FC, Chipukizi na URA ya Uganda.
Kundi B linaundwa na timu za Simba SC, Jamhuri SC, APR ya Rwanda na Singida Fountain Gate.
Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya michuano ya msimu huu, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Mahmoud Jabir, amesema hii itakuwa ni moja kati ya michuano mikubwa na bora kushuhudiwa kutokana na aina ya timu ambazo wameziandaa kushiriki.
"Tunatarajia kuwa na michuano bora sana msimu huu kwasababu kwanza tumeongeza timu lakini pia tumealika timu zenye ushindani kutoka nje," amesema.
Aidha alibainisha mechi zote katika michuano ya msimu huu zitachezwa katika Uwanja wa Amani visiwani humo.
Michuano ya Mapinduzi msimu huu itakuwa ni sehemu ya shamrashamra ya kusherehekea miaka 60 tangu Mapinduzi Matakatifu ya Zanzibar.
Msimu uliopita, Mlandege ilivunja mwiko kwa timu za Zanzibar kutofanya vizuri kwenye michuano hiyo baada ya kuibuka na taji kwa kuifunga Singida FG katika mchezo wa fainali uliochezwa Januari 13.