Bao la Bajana laweka rekodi

LIGI KUU Bao la Bajana laweka rekodi

Zahoro Mlanzi • 16:03 - 12.12.2023

Kiungo huyo wa Azam FC amefunga bao sekunde ya 54 ikiwa ndio bao lililofungwa mapema zaidi katika ligi hiyo

Kiungo wa timu ya Azam FC na timu ya Taifa ya Tanzania, Sospeter Bajana, ameweka rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi msimu huu alilofunga kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Jumatatu na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Bao hilo alilifunga katika sekunde ya 54 ya mchezo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Pascal Msindo na kuachia shuti kali la umbali wa zaidi ya mita 25 na kumshinda mlinda lango wa JKT Tanzania, Ismail Salehe.

Kabla ya bao la Bajana, mabao mawili yalikuwa na rekodi ya kufungwa mapema zaidi katika dakika ya kwanza ni la Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji aliyewafunga Tabora United na Awesu Awesu wa KMC aliyewafunga Mashujaa.

Baada ya kufungwa bao hilo la mapema, JKT Tanzania, walisawazisha katika dakika ya 37 kupitia kwa Najimu Magulu baada ya kipa wa Azam, Ali Ahamad kupishana mawasiliano na walinzi wake na kuliacha lango wazi kwa bao safi kuingia.

Kipindi cha pili, dakika ya 81, winga wa Azam, Idd Seleman aliifungia timu yake bao la ushindi akimalizia kazi nzuri ya Edward Manyama katika upande wa kulia.

Ushindi huo, umezidi kuwakita Azam kileleni wakifikisha alama 28 baada ya kushuka uwanjani mara 12 na unakuwa ni ushindi wa tano mfululizo tangu walipofungwa nyumbani na Namungo.