Benchikha 'alia' na mastraika wake kutofunga mabao mengi

KANDANDA Benchikha 'alia' na mastraika wake kutofunga mabao mengi

Zahoro Mlanzi • 20:49 - 11.12.2023

Kocha huyo wa Simba amesikitishwa na wachezaji wake kutofunga mabao mengi katika michuano ya kimataifa

Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amewatupia lawama washambuliaji wake kwa kukosa umakini mbele ya goli kiasi cha kufanya timu hiyo kukosa matokeo ya ushindi katika michezo ya kimataifa msimu huu.

Washambuliaji wa Simba ambao mara kadhaa huwa wanapata muda mwingi wa kucheza ni pamoja na Jean Baleke na Moses Phiri huku pia nahodha wa kikosi hicho, John Bocco naye akiwa anatumika kwa nyakati fulani.

Akizungumza mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam wakitokea nchini Morocco, Benchikha, amesema anakubali wachezaji wake wote wanajituma uwanjani lakini alikiri kuwa takwimu katika idara ya ushambuliaji haimridhishi.

"Katika hatua hii ya makundi tumecheza mechi tatu, dhidi ya Asec Mimosa, Jwaneng Galaxy na Wydad lakini tumefunga bao moja tu tena kwa njia ya mkwaju wa penalti," amesema Benchikha.

Ameendelea hiyo sio hali nzuri lakini atajitahidi kulifanyia kazi jambo hilo ili lisiendelee kutokea.

Aidha Benchikha amewamwagia sifa wachezaji wake wa idara ya kiungo ambapo amesema wamekuwa wakimvutia katika mechi zote walizocheza.

"Viungo wangu wanafanya kazi nzuri, wanatawala mchezo na kusambaza mipira kwa ustadi wa hali ya juu, ama hakika ninajivunia nao," amesema.

Katika hatua nyingine, Benchikha amemtupia lawama mwamuzi wa kati ambaye amecheza mchezo wao dhidi ya Wydad ambapo akidai alifanya makosa kwa kuongeza dakika tatu lakini akachezesha kwa dakika nyingi zaidi ya alizoongeza.

Katika mchezo huo, Simba licha ya kuwa walicheza kwa zaidi ya dakika 90 matokeo yakiwa ni 0-0 lakini walijikuta wakiruhusu bao katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza lililofungwa na Zakaria Draoui.

Kwa matokeo hayo Simba sasa wametupwa hadi mkiani katika Kundi B ambapo wamebaki na alama 2 huku anayeongoza kundi NI Asec akiwa na alama 7.

Jwaneng wao wapo nafasi ya pili na alama 4 huku Wydad wakiwa nafasi ya tatu na alama zao 3 baada ya kupata ushindi wao wa kwanza.

Mchezo unaofuata wa Simba utakuwa ni wa marudiano dhidi ya Wydad ambao utapigwa Desemba 19 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Tags: