Benchikha atamba kujua siri za Wydad Casablanca

KANDANDA Benchikha atamba kujua siri za Wydad Casablanca

Na Zahoro Mlanzi • 19:34 - 08.12.2023

Kocha huyo mpya wa Simba SC ataiongoza timu yake kesho kuumana na timu hiyo

Kocha Mkuu wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema anaifahamu Wydad Casablanca na hivyo ana matumaini ya kufanya vizuri dhidi yao.

Hayo ameyasema Ijumaa ikiwa ni siku moja kabla ya Simba kushuka dimbani nchini Morocco kwenye Mji wa Marekech kukabiliana na Wydad kwenye mchezo wa tatu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Benchikha ambaye huo utakuwa ni mchezo wa pili kwake amewahi kufundisha nchini Morocco kwenye timu ya RS Berkane lakini pia kipindi cha nyuma amewahi kuwa kocha wa Wydad.

"Mchezo utakuwa mgumu kwasababu Wydad ni timu kubwa na yenye uzoefu, lakini sisi tupo hapa kutafuta alama ambazo naamini tutazipata, ninawajua vizuri wapinzani wetu na ninajua utakuwa mchezo mzuri," amesema.

Mchezo huo utakuwa ni wa pili kwa kocha Benchikha ambaye alijiunga na Simba wiki iliyopita. Hata hivyo huu utakuwa ni mchezo watatu kwa Simba katika hatua hii.

Msimamo wa Kundi B, unaonesha Wydad wanaburuza mkia wakiwa hawana alama huku Simba wao wakiwa wamevuna alama mbili katika michezo yao miwili iliyopita na Asec Mimosa na Jwaneng Galaxy wote wapo juu wakiwa na alama nne katika kundi hilo.

Pia Kiungo wa timu hiyo, Fabrice Ngoma, amesema wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo na wanahitaji kufanya dhidi ya Wydad ili wajiweke katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

"Sisi tupo tayari kwa mchezo, tumefanya maandalizi mazuri na tunahitaji kupambana uwanjani kwa ajili ya timu," amesema.

Simba itaumana na Wydad kesho kuanzia saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Tags: