Benchikha kutumia mashindano ya Mapinduzi Cup kuwajua nyota wake

KANDANDA Benchikha kutumia mashindano ya Mapinduzi Cup kuwajua nyota wake

Na Zahoro Mlanzi • 18:25 - 02.01.2024

Kocha huyo alijiunga na Simba Oktoba, mwaka jana kuchukua mikoba ya Mbrazil, Roberto Oliviera 'Robertinho, hivyo hajapata muda mwingi wa kuiona timu yake

Kocha wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema ataendelea kuwatumia wachezaji wake wa kikosi cha kwanza katika michuano ya Mapinduzi Cup lengo ikiwa ni kuwatambua vizuri zaidi.

Hayo ameyasema wakati akijiandaa kukabaliana na Singida Fountain Gate katika mchezo wao wa pili wa Kundi B wa michuano hiyo unaotarajia kuchezwa kesho saa 2:15 usiku.

Benchikha amesema ataitumia michuano hiyo kwa lengo la kukisuka kikosi chake vizuri hasa ukizingatia alikosa muda wa kufanya hivyo kutokana na ratiba aliyoikuta wakati anajiunga na Simba mwanzoni mwa Desemba.

"Michuano hii itakuwa ni sehemu nzuri ya mimi kuingiza baadhi ya mbinu zangu kwa wachezaji waliopo wa kikosi cha kwanza, nitatumia vizuri ratiba hii kuwapa nafasi muhimu kila mchezaji," amesema.

Katika mchezo wao wa kwanza Simba, ilipata ushindi wa mabao 3-1 mbele ya JKU na kwenye mchezo huo Benchikha ameonekana kupanga idadi kubwa ya wachezaji wanaotumainiwa katika kikosi cha kwanza.

Mbali na na mechi hiyo, lakini pia saa 10 alasiri kutashuhudiwa mchezo mwingine wa kundi hilo ambapo APR kutoka Rwanda itacheza na JKU ambao tayari wameshatupwa nje ya michuano kutokana na kufungwa kwenye mechi zao mbili za awali.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Klabu ya Simba, umetangaza kuiunga mkono Serikali ya Zanzibar katika sekta ya utalii ambapo umesema kuanzia mchezo wao wa leo watavaa jezi yenye nembo ya ‘Visit Zanzibar’.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Ally amesema Simba wameona ni jambo jema kuinua sekta ya utalii kwa kutumia jina lao kutangaza vivutio mbalimbali ambavyo vinapatikana Zanzibar.

Ameongeza wanatarajia siku zao za mapumziko kutembelea kwenye sehemu mbalimbali za utalii ambazo hasa hazipewi kipaumbele ili kuhabirisha umma kuhusu vivutio hivyo.

Tags: