Bosi huyo ametoa kauli hiyo wakati timu yake ikijiandaa na mechi zaidi ya tatu kabla ya mwaka mpya kuingia
Klabu ya soka ya Yanga, imetamba msimu huu itatetea makombe yote iliyotwaa msimu uliopita kutokana na ubora wa kikosi chao.
Kauli hiyo, imetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu 'CEO' wa klabu hiyo, Andre Mtine, wakati timu hiyo ikijiandaa na mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Msimu uliopita Yanga, imetwaa ubingwa wa ligi na Kombe la FA kama walivyofanya pia msimu wa nyuma yake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mtine amesema maandalizi yanaendelea vizuri chini ya Kocha, Miguel Gamondi lakini wao kama uongozi wapo karibu na kocha huyo ili kumuwezesha kwa mahitaji yake.
Mtine amesema licha ya ugumu wa michuano ya msimu huu lakini wao hawana wasiwasi na ubora wa kikosi chao.
Amesema ndani ya mwezi huu wamekuwa na ratiba ngumu lakini wana imani ya kumaliza salama mechi zao zote.
"Timu yetu ina wachezaji bora na inaandaliwa vizuri, sisi kama uongozi tunaimani ya kufanya vizuri na tuna nia ya kutetea mataji yetu ambayo tuliyashinda msimu uliopita," amesema.
Mbali ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar lakini pia Yanga wana mchezo mwengine muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama SC ambao unatarajiwa kuchezwa Jumatano.
Wakati huo huo, uongozi wa Yanga, unatajwa kukamilisha dili la mchezaji wa JKU ya Zanzibar, Shekhan Ibrahim, 18.