Diarra aongeza mzuka kikosini Yanga SC

KANDANDA Diarra aongeza mzuka kikosini Yanga SC

Na Zahoro Juma • 12:00 - 14.02.2024

Ni baada ya kuanza mazoezi na wenzake akitoka kucheza robo fainali ya michuano ya AFCON

Baada ya kuanza ligi kwa kusuasua hasa katika eneo la milingoti mitatu, hatimaye Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, ameshusha presha baada ya kurejea kikosini kwa kipa wake namba moja, Djigui Diarra.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa klabu ya Yanga, Diarra amerejea nchini tayari kwa kuendelea na majukumu yake ndani ya timu hiyo ambayo kwasasa ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na alama 40.

“Mlinda lango wetu namba moja, Djigui Diarra amerejea nchini na tayari amejiunga na wenzake kwa ajili ya maanadalizi ya mechi zinazofuata,” imesomeka taarifa ya Yanga.

Diarra alikuwa akishiriki michuano ya Afcon akiwa na timu yake ya Mali ambapo alicheza michezo yote mitano na kujiondokea na ‘clean sheet’ tatu katika michezo hiyo hadi walipotolewa katika hatua ya robo fainali na wenyeji Ivory Coast.

Wakati Diarra akiwa katika michuano ya Afcon, jukumu kulinda milingoti mitatu ya Yanga lilibaki kwa makipa wawili wazawa Abuutwalib Mshery na Metacha Mnata.

Hata hivyo kiwango kilichooneshwa na makipa hao waliochiwa jukumu la kulinda lango la Yanga hakikuwa cha kuridhisha kwa kiasi kikubwa kwani kwa pamoja walifanikiwa kuvuna ‘clean sheet’ mbili tu katika michezo mitano.

Mshery aliaminiwa katika michezo mitatu dhidi ya Hausang, Kagera Sugar ana Mashujaa ambapo alifanikiwa kupata ‘clean sheet’ katika mechi moja tu dhidi ya Kagera Sugar.

Kwa upande wake, Metacha yeye alidaka mechi dhidi ya Dodoma Jiji ambapo Yanga ilishinda 1-0 lakini katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons licha ya kuwa hakuruhusu bao lakini alitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Kurejea kwa Diarra ambaye hadi ligi inasimama alikuwa ni mmoja wa makipa aliyekuwa akiongoza kwa ‘clean sheet’ ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga lakini hasa Kocha Gamondi ambaye alikuwa anakuna kichwa kuhusu eneo hilo muhim uwanjani.

Timu ya Yanga hadi sasa katika ligi hiyo imeruhusu mabao nane katika ligi lakini matatu yameingia katika mechi tatu za hivi karibuni.

Yanga inakabiliwa na mechi mwishoni mwa wiki hii dhidi ya KMC katika muendelezo wa ligi kuu bara mzunguko wa pili huku pia wakiwa na mchezo wa Kombe la Azam Sports Federation Cup dhidi ya Polisi Tanzania.

Tags: