Nyota huyo alichelewa kujiunga na timu yake ya Yanga akitokea katika michuano ya AFCON alipokuwa akiitumikia Burkina Faso
Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema kurejea kwa Kiungo mshambuliaji wake, Stephane Aziz Ki, kutaongeza makali katika safu yake ya ushambuliaji.
Aziz Ki amekosekana katika mechi nne za awali kutokana na majukumu ya timu ya yake ya Taifa ya Burkina Faso ambayo iliishia hatua ya 16 Bora ya michuano ya AFCON iliyomalizika mwishoni mwa wiki.
Kiungo huyo, pia ndiye kinara katika upachikaji mabao ndani ya Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 10 hadi sasa.
Akizungumza na Pulse Sports, Gamondi, amejivunia kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo huku timu yake ikiwa kileleni kwenye msimamo.
Gamondi amesema haikuwa kazi rahisi hasa ukizingatia ugumu wa ligi ya msimu huu kwa sababu timu nyingi zipo katika kiwango kizuri cha ushindani.
"Najivunia kwa wachezaji wangu kuweza kupambana na kumaliza mzunguko huu wa kwanza tukiwa tunaongoza ligi, hii haikuwa kazi rahisi hasa ukiangalia ushindani uliopo kutoka kwa timu ambazo tunachuana nazo," amesema Gamondi.
Yanga kwa sasa imejikita kileleni wakifikisha alama 40 baada ya kucheza mechi 15, hiyo Ikiwa na maana katika mzunguko huo wa kwanza wamepoteza alama tano.
Aidha kocha huyo amekiri amejisikia vizuri baada ya kiungo wake Ki kurejea tena uwanjani mara baada ya kushiriki Afcon.
Amesema Ki, licha ya kuchelewa kurudi na kujiunga na timu lakini baada ya kuanza kucheza, ameanza kuwaonesha kitu ambacho walikuwa wanakosa kutoka kwake.