Kocha huyo wa Yanga ametoa kauli hiyo baada ya wachambuzi wa soka nchini Tanzania kushauri awe anabadili kikosi chake
Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema halazimiki kubadilisha kikosi chake cha kwanza kwakuwa bado kinafanya vizuri.
Hayo ameyasema jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuelekea mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex.
Gamondi amesema kikosi anachopanga kinatokana na kile anachoona mazoezini hivyo kila mchezaji anatakiwa kupigania nafasi yake kwenye mazoezi.
"Sitoi nafasi kwa upendeleo, napanga timu kulingana na mazoezi tunayofanya na ndio maana silazimiki kubadilisha mara kwa mara kwa sababu timu inafanya vizuri," amesema.
Kuhusu mechi dhidi ya Mtibwa, Gamondi amesema licha ya kuwa timu hiyo ipo chini kwenye msimamo lakini hawatawadharau.
Amesema mechi zote kwenye ligi ni ngumu hivyo wataingia katika mechi hiyo wakiwa na tahadhari zote.
Yanga wanaingia uwanjani kucheza mechi hiyo ikiwa ni mchezo wao wa 10 msimu huu.
Kwasasa timu hiyo ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 24 nyuma ya Azam FC ambao wanaongoza ligi wakiwa na alama 28 na wamecheza mechi tatu zaidi.