Gamondi sasa kupitisha 'fagio' Yanga SC

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi (kushoto), wakijadili masuala mbalimbali na wasaidizi wake

KANDANDA Gamondi sasa kupitisha 'fagio' Yanga SC

Na Zahoro Mlanzi • 22:38 - 12.01.2024

Hatua hiyo itafikiwa baada ya Kocha huyo wa Yanga, kuwasilisha ripoti baada ya kutolewa michuano ya Mapinduzi Cup

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ametumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi kufanya tathimini ya kikosi chake na sasa kuna maamuzi mazito yatatolewa hivi karibuni.

Yanga imeondolewa katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya APR ya nchini Rwanda mchezo uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kocha huyo katika mashindano hayo, aliwapa nafasi ya kucheza wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika na vijana wa U-20 aliowapandisha kwa ajili ya kutathimini viwango vyao kabla ya kuchukua maamuzi ya kuwakata katika dirisha dogo.

Akizungumza na Pulsesports, Gamondi amesema malengo ya kushiriki mashindano hayo, yametimia kwa kiwango kikubwa ambayo ya kwanza yalikuwa ni kuwatambua wachezaji wasiokuwa na sifa ya kubakia Yanga.

Ameongeza amepanga kukabidhi ripoti ya wachezaji hao kwa uongozi hivi karibuni ikiwa ni siku chache tangu watoke kuondolewa katika mashindano hayo.

“Licha ya kuondolewa katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Mapinduzi, lakini kwangu nimefurahia kuona malengo ya ushiriki wa mashindano haya kukamilika," amesema Gamondi.

“Hivyo malengo yangu yametimia, na kinachofuata hivi ni utekelezaji wa viongozi baada ya mimi kukamilisha ripoti yangu".

Kupitia dirisha dogo la usajil, Yanga imekamilisha usajili wa mastaa wawili na kuwatangaza ambao ni Shekhani Ibrahim na kiungo wa kimataifa wa Ghana, Augustine Okrah.

Tags: