Hatukuwa na aina ya maandalizi ambayo tuliyataka, tumetoka kucheza mchezo mgumu dhidi ya Simba kisha tumesafiri kuja Tanga
Kocha wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema licha ya kikosi chake kuwa na uchovu lakini watapambana kuondoka na alama tatu dhidi ya Coastal Union.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, unatarajiwa kuchezwa kesho kuanzia saa 12.30 jioni uwanjani Mkwakwani, Tanga.
Yanga itashuka uwanjani ikitoka kuitandika Simba mabao 5-1 huku Coastal yenyewe ikitoka suluhu Namungo FC.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Gamondi amesema licha ya uchovu ambao wanao wachezaji wake lakini wapo tayari kuendelea kutoa burudani kwenye mchezo huo.
Amesema maandalizi hayakuwa makubwa kuelekea mchezo huo kwasababu ya ratiba kubana lakini anashukuru wachezaji wake wapo tayari.
"Hatukuwa na aina ya maandalizi ambayo tuliyataka, tumetoka kucheza mchezo mgumu dhidi ya Simba kisha tumesafiri kuja Tanga, maandalizi tumefanya kidogo jana na leo," amesema.
"Hata hivyo nashukuru wachezaji wangu ni hodari wameweza kuhimili hali hii na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huu ambao nadhani utakuwa mgumu," amesema.
Yanga wanacheza na Coastal ambao hawapo vizuri kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa kwenye nafasi ya 13 kwa alama 7 baada ya kushuka dimbani mara 8 na kupata ushindi kwenye mchezo mmoja tu.
Kikosi cha Coastal Union kipo chini ya Kocha Fikiri Elias ambaye amechukua nafasi ya Kocha, Mwinyi Zahera ambaye amewekwa pembeni kutokana na matokeo ambayo si ya kuridhisha.
"Yanga ni timu nzuri na wametoka kupata ushindi mzuri ambao unawaongezea morali, hata hivyo mimi nimewaandaa wachezaji wangu kwa ajili ya mchezo mzuri hiyo kesho," amesema Kocha Elias.