JKT Queens kuanza na Mamelodi Ligi ya Mabingwa Afrika

© Kwa Hisani

KANDANDA JKT Queens kuanza na Mamelodi Ligi ya Mabingwa Afrika

Zahoro Mlanzi • 19:30 - 16.10.2023

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Novemba 5 kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake, timu ya JKT Queens, itaanza kuumana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya Kundi A.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Novemba 5 kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), michuano hiyo itafanyika hadi Novemba 19.

Mchezo wa awali wa ufunguzi utazikutanisha Atletico Abdijan itakayoumana na Sporting Club Casablanca kwenye Uwanja wa Korhogo Ahmadou Gon Coulibaly.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, JKT Queens itashuka tena uwanjani dhidi ya Atletico Novemba 8 na kisha itamaliza na Sporting Club Casablanca Novemba 11.

Akizungumzia ratiba hiyo, Ofisa Habari wa timu ya JKT Queens, Masau Bwire, amesema imekaa vizuri na kwamba wana imani ya kufika mbali.

"Tunaendelea na maandalizi yetu kwa ajili ya michuano hiyo kwa kucheza mechi mbalimbali za kirafiki, tuna imani kwa ratiba hiyo tumeanza kuiona njia ya robo fainali," ametamba Bwire.