JKT Queens yapigwa 2-0 na Mamelodi, Kocha afunguka

KANDANDA JKT Queens yapigwa 2-0 na Mamelodi, Kocha afunguka

Na Zahoro Mlanzi • 18:58 - 06.11.2023

Tumecheza vizuri lakini wapinzani wetu walikuwa bora na hasa walituzidi katika uzoefu

Licha ya kupoteza kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mamelodi Sundowns Ladies kwa 2-0, Kocha wa timu ya JKT Queens, Ester Chabruma, bado ana imani na kikosi chake ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake.

Katika mchezo huo, ambao ulichezwa usiku wa kuamkia Jumatatu nchini Ivory Coast, JKT Queens walikubali kichapo hicho huku mabao ya Mamelodi yakifungwa na Lebogang Ramalepe na Refilwe Tholakele.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha Chabruma, amezungumza kwa simu kutoka Ivory Coast, akisema wamecheza vizuri lakini wapinzani wao walikuwa bora na hasa waliwazidi katika uzoefu.

Hata hivyo amekiri nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo bado wanayo kwani wana michezo miwili ambayo watajipanga kufanya vizuri.

"Kikosi chetu hakijacheza vibaya ila ni makosa tu ndio yaliyofanya tufungwe, wapinzani wetu ni bora na wana uzoefu mkubwa tofauti na sisi," amesema.

'Nafasi bado ipo kwa hivyo ni jukumu letu kufanyia kazi mapungufu yetu ili tuweze kurekebisha katika mechi zijazo," amesema.

JKT watashuka tena uwanjani Jumatano kwa ajili ya mchezo wa pili ambao watacheza dhidi ya wenyeji Athletico Abidjan mchezo utakaopigwa saa 11.

Mchezo mwingine katika kundi hlao la A, timu za Athletico Abidjan na Sporting Casablanca ya Morocco zikitoka sare ya 1-1.

Tags: