JKT Queens yapokwa pointi 5 na faini sh. milioni 3

KANDANDA JKT Queens yapokwa pointi 5 na faini sh. milioni 3

Na Zahoro Juma • 15:00 - 04.02.2024

Timu hiyo ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara

Klabu ya JKT Queens, inayoshiriki Ligi ya Wanawake ya Tanzania Bara, imeshushiwa rungu la kunyang'anywa alama tano na kutozwa faini ya sh. milioni 3 kwa kosa la kushindwa kutokea katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kucheza mechi ya ligi hiyo dhidi ya Simba Queens.

Mbali na rungu hilo kwa JKT Queens lakini pia Katibu Mkuu wa timu hiyo, Duncan Maliyabwana, amesimamishwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi 12.

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni za mashindano hayo 32. 1-3. Klabu ya Simba Queens wenyewe imepewa alama 3 na mabao matatu kama inavyoelekeza kanuni namba 18:45.

Tukio hilo lilitokea Januari 8, mwaka huu ambapo JKT Queens na Simba Queens walitarajiwa kucheza mchezo wa ligi lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida timu hizo kila mmoja alifika katika uwanja tofauti.

Wenyeji JKT Queens wao walikwenda katika Uwanja wa Meja Jenarali Isamuhyo ambapo mara nyingi hutumia uwanja huo kwa mechi zao za nyumbani. Nao wageni wa mchezo Simba Queens wao walikwenda kwenye Uwanja wa Azam Complex pamoja na waamuzi kitu ambacho kilisababisha mchezo huo kutofanyika.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka Kamati ya Soka la Wanawake, JKT Queens imekuwa inayo taarifa kuhusu mchezo huo kufanyika katika Uwanja wa Azam Complex.

"Kamati imejiridhisha kuwa JKT Queens walikuwa na taarifa ya uwanja kabla hata siku ya mchezo na hata ilipofika siku ya mchezo Mwenyekiti wa kikao alikumbushwa kuhusu uwanja na muda wa mchezo katika kikao cha maandalizi," imesomeka taarifa ya kamati.

Kwa kitendo cha kukatwa alama 5 maana yake watabakiwa na alama 16 na imeshuka hadi nafasi ya pili nyuma ya Simba ambao kwasasa wana alama 19 lakini wakiongeza alama zao tatu za mezani watakuwa na alama 22.

Tags: