Straika huyo amesajiliwa na timu hiyo akitokea timu ya Zhenis ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Kazakhstan
Mshambuliaji mpya wa timu ya Simba SC, Pa Omar Jobe, amesema ametoka Ulaya kuja Tanzania kwa ajili ya kuja kufanya kazi moja tu ya kufunga mabao.
Hayo ameyasema ikiwa ni saa chache baada ya kufunga bao lake la kwanza akiwa na jezi ya Simba katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tembo FC katika mchezo wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) uliopigwa jana.
Mchezaji huyo raia wa Gambia, ameingia kipindi cha pili na alifunga bao lake hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Saido Ntibanzokiza.
Akizungumza na Pulsesports, Jobe amesema anajua kilichomtoa Ulaya na kurudi kucheza Afrika kwenye timu ya Simba kuwa ni kufunga mabao kwahiyo aliwataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi naye.
"Nimeacha kucheza mpira Ulaya nimekuja hapa najua kilichonileta, najua mashabiki wanataka matokeo na wanataka mabao kutoka kwangu, kazi hiyo ninaiweza," amesema Jobe.
Aidha mchezaji huyo amekiri bado hajawa katika kiwango chake kutokana na kuwa na siku chache tangu atue nchini lakini pia amekuta hali ya hewa tofauti na alipotoka hivyo atahitaji muda wa kuzoea mazingira.
Jobe alikuwa akiichezea timu ya Zhenis ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Kazakhstan. Katika mechi 25 alizocheza msimu uliomalizika alifunga mabao 13.
Mbali na Jobe lakini Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha pia aliwapa nafasi ya kucheza wachezaji wake wote wapya aliowasajili kwenye dirisha dogo akiwemo Freddy Michael, Ladack Chasambi na Saleh Karabaka.
Wakati huo huo, kikosi cha Simba SC, kimetua salama mkoani Kigoma na kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ambapo itacheza na wenyeji wao Mashujaa FC.
Mchezo huo unatarajia kuchezwa Uwanja wa Lake Tanganyika wakati Simba wakisaka alama tatu muhimu za kuwarejesha katika mstari wa kuwania taji msimu huu.