Kamati Mapinduzi Cup yakiri kosa kutoa kona Simba

Kipa wa timu ya Simba SC, Ally Katoro, akiokoa moja ya mikwaju ya penalti wakati wa mechi yao dhidi ya Singida FG

KANDANDA Kamati Mapinduzi Cup yakiri kosa kutoa kona Simba

Na Zahoro Mlanzi • 19:00 - 11.01.2024

Kona hiyo uliyopigwa ndani ya dakika 6 za nyongeza ndio iliyosababisha Simba SC kusawazisha bao mbele ya Singida FG

Baada ya mijadala ya muda mrefu katika vijiwe mbalimbali vya soka, hatimaye Kamati ya Waamuzi wa Zanzibar, imemaliza utata ikisema Mwamuzi wa mchezo kati ya Singida FG na Simba SC, Nasri Salum ‘Msomali’, hakuwa sahihi kuwapa shambulizi la kona Simba.

Kauli hiyo imekuja baada ya Singida FG kutolewa katika michuano ya Mapinduzi Cup na Simba kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya dakika 90 kufungana bao 1-1.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Waziri Shekha, baada ya kikao kilichofanyika jana na kupitia kwa ufanisi waligundua Msomali na waamuzi wasaidizi wake hawakuwa sahihi kutoa uamuzi wa kona kwa Simba.

Shekha amesema kosa hilo ni la kibinadamu kwani waamuzi nao hufanya makossa ambapo wamebaini ndio kosa pekee alilofanya Msomali katika michuano hiyo.

Wakati huohuo, Kocha Msaidizi wa timu ya Simba, Seleman Matola, amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi dakika ya mwisho na kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo.

Akizungumza na Pulsesports, Matola amesema ulikuwa mchezo mgumu kwa pande zote mbili na kama wachezaji wake wangekata tamaa basi kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza mchezo.

Amesema Singida ni timu nzuri na yenye ushindani hivyo wao kupata matokeo ya ushindi katika mchezo huo ni jambo la kujivunia.

Katika mchezo huo, Singida FG ilipata bao la uongozi mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao, Mkenya Elvis Rupia ambaye alifikisha bao lake la tano kwenye michuano hiyo.

Hata hivyo Simba, ilichomoa bao hilo dakika za majeruhi kipindi cha pili kupitia kwa kiungo wao, Fabrice Ngoma na kufanya mchezo huo uamuliwe kwa njia ya mikwaju ya penalti.

Simba sasa wanalisaka taji hilo baada ya kulipoteza mwaka jana ambapo Mlandege walilitwaa mbele ya Singida FG ambapo fainali itapigwa Januari 13.

Tags: