Kocha Dabo afunguka ubingwa unavyopatikana

KANDANDA Kocha Dabo afunguka ubingwa unavyopatikana

Na Zahoro Juma • 21:32 - 07.02.2024

Dabo amepewa majukumu ya kuinoa timu ya Azam FC ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga SC kwa tofauti ya alama 2

Kocha Mkuu wa kikosi cha Azam FC, Yusuph Dabo, amesema timu yake imejiwekea malengo ya kuwania ubingwa kabla hata ya Ligi Kuu Bara kuanza msimu huu.

Hayo ameyasema wakati akifanya mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ili timu kuwa bingwa mipango haiwezi kufanyika wakati ligi inaendelea.

"Tulipanga tangu wakati wa maandalizi ya msimu, huwezi kuwania ubingwa kwa kusubiri kuona msimamo unavyokuwa katikati ya ligi, hili ni wazo ambalo unatakiwa kuliweka mwanzoni na kisha msimu ukianza unaanza kulipigania," amesema.

Ameendelea kusema kazi yao kama benchi la ufundi ni kuendelea kujenga kikosi chao na kuwapa mbinu wachezaji ambazo zitawasaidia wao kutimiza malengo yao waliyojiwekea msimu huu.

Azam hawajashinda taji la ligi kwa takribani miaka 11 tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2013.

Hata hivyo msimu huu, wanaonekana kuwa mstari wa mbele katika kuliwania taji hilo wakiwa wanaonekana kuwa na kikosi chenye tija na kinachoweza kuwapatia mafanikio.

Wakati huo huo, kikosi cha Azam kimetua salama jijini Mwanza tayari kwa ajili ya kuikabili Simba kwenye mchezo wa ligi hiyo ambao unatarajia kufanyika Ijumaa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Mchezo huo wa kiporo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini unatarajia kubeba taswira ya ubingwa msimu huu kwa timu zote mbili ambazo hadi sasa zinawania kuwavua taji Yanga.

Yanga kwasasa ipo kileleni ikiwa na alama 34 akifuatiwa na Azam wenye alama 31 na Simba ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 29 na wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Tags: