Kocha mpya Simba SC atua na wasaidizi wake

LIGI KUU Kocha mpya Simba SC atua na wasaidizi wake

Na Zahoro Mlanzi • 08:00 - 28.11.2023

Kibarua chake cha kwanza kitakuwa dhidi ya Janweng Galaxy ya Botswana mchezo utakaopigwa Desemba 2

Kocha mpya wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha raia wa Algeria, amewasili nchini Tanzania tayari kuanza majukumu mapya ndani ya timu hiyo.

Benchikha anatarajiwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu ndani ya timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika mtandao wa kijamii wa klabu hiyo, Benchikha ametua nchini na jopo la makocha wengine wawili.

Taarifa hiyo imewataja makocha hao wengine ni Farid Zemiti ambaye atakuwa Kocha Msaidizi pamoja na Kamal Boujdjenane ambaye ni Kocha wa Viungo.

Benchikha ataanza maisha mapya ndani ya Klabu hiyo, akirithi mikoba ya Mbrazil, Roberto Oliviera 'Robertinho' ambaye alitimuliwa baada ya kufungwa mabao 5-1 na Yanga SC mchezo uliopigwa Novemba 5.

Kocha huyo kibarua chake cha kwanza kitakuwa ugenini dhidi ya Janweng Galaxy ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi utakaopigwa Desemba 2 nchini humo.

Ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi katika ngazi za juu katika soka la Afrika.

Anajiunga na Simba akiwa anatokea Klabu ya USM Alger ambayo msimu uliopita aliwasaidia kushinda taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwafunga Yanga katika mchezo wa fainali.

Pia Benchikha ameisaidia USM Alger kushinda ubingwa wa Super Cup ambapo aliwafunga Al Ahly katika mchezo uliofanyika Saudi Arabia.

Ameachana na miamba hao wa Algeria mwanzoni tu mwa msimu huu baada ya kushindwa kuelewana na viongozi katika baadhi ya mambo.

Tags: