Kocha Roberto Oliviera asema ushindi wao dhidhi ya Tanzania Prisons umeonyesha ukubwa wa Simba SC

Kocha Roberto Oliviera asema ushindi wao dhidhi ya Tanzania Prisons umeonyesha ukubwa wa Simba SC

Zahoro Mlanzi • 20:00 - 06.10.2023

Simba SC waliwapiga Tanzania Prisons mabao matatu kwa moja na Kocha wa Simba ana unahakika ushindi huo umeonyesha ukubwa na ubora wa timu yake.

Kocha Mkuu wa timu ya Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’, amesema katika ushindi wa mabao 3-1 walioupata dhidi ya Tanzania Prisons umeonyesha ukubwa na ubora wa timu yake.

Ushindi huo umeifanya timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kujikusanyia alama 12 ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 10 na Yanga alama 9.

Akizungumza na Pulsesports baada ya kurejea jijini Dar es Salaam wakitokea Mbeya, Robertinho amesema licha ya kufungwa bao la mapema wachezaji hawakuchanganyikiwa badala yake walitulia na kucheza katika mipango ile ile waliyokuwa wamepanga na huo ndio ukubwa.

Robertinho amewapongeza wachezaji kwa jinsi walivyocheza soka safi lililowapa ushindi mnono na alama tatu muhimu.

“Mchezo wa huu umeonyesha daraja la Simba lipo juu, tulifungwa bao la mapema lakini halikututoa mchezoni tulimiliki mpira kama kawaida tukasawazisha na kuongeza.

Mara zote nasisitiza tunapaswa kucheza soka safi na kushinda na ndicho kilichotokea, nawapongeza wachezaji wangu kwa kazi kubwa waliyofanya,” amesema Robertinho.

Amesema wachezaji wake siku zote hucheza kwa kuburudika bila ya kuwa na mawazo wakiamini watapata matokeo mazuri wakati wowote.

Kuhusu mashabiki waliojitokeza kwa wingi Robertinho amesema: “Wamekuwa wakitupa sapoti na mara zote wamekuwa upande wetu, tunawashukuru sana kwa hili.”

Timu hiyo kwa sasa inajiandaa na mchezo mwingine wa ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate utakaopigwa Jumapili Uwanja wa Liti, mkoani Singida.

Baada ya mchezo huo, Simba itakuwa ikijiwinda dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa African Super League utakaopigwa Oktoba 20.

Tags: