Kocha wa Simba SC, Mayele watinga Tatu Bora

TUZO ZA CAF Kocha wa Simba SC, Mayele watinga Tatu Bora

Na Zahoro Mlanzi • 16:22 - 07.12.2023

Tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Desemba 13 nchini Morocco

Kocha Mkuu wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha na mshambuliaji wa zamani wa timu ya Yanga SC, Fiston Mayele, wameingia Tatu Bora katika kinyang'anyiro cha kuwania Tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Benchikha ambaye amejiunga na Simba mwanzoni mwa wiki iliyopita kurithi mikoba iliyoachwa wazi na Roberto Oliviera 'Robertinho', ameingia katika hatua hiyo baada ya kupata mafanikio na timu yake ya zamani ya USM Alger ambapo aliwaongoza kushinda ubingwa wa Shirikisho Afrika kwa kuifunga Yanga kwenye mchezo wa fainali.

Mbali na ubingwa huo lakini pia Benchikha ameshinda ubingwa wa Super Cup msimu huu kwa kuifunga Al Ahly kwenye mechi iliyochezwa nchini Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), katika tuzo hiyo, Benchikha atakabiliana uso kwa uso na Kocha wa timu ya Taifa ya Senegal, Aliou Cisse ambaye ni mshindi wa taji la Afcon 2022.

Kocha wa tatu katika kinyang'anyoiro hicho ni Walid Regragui ambaye ni Kocha wa timu ya Taifa ya Morocco na aliongoza timu hiyo kuvunja rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Qatar Novemba, 2022.

Kwa upande wake, Mayele ambaye kwasasa anakipiga na Klabu ya Pyramids ya nchini Misri, anawania Tuzo ya Mchezaji Bora wa ndani dhidi ya Peter Shalulile wa Mamelodi Sundowns na Percy Tau wa Al Ahly.

Mayele akiwa na Yanga msimu uliopita, ameibuka Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho akiwa na mabao 6 na pia Mfungaji Bora wa Ligi Kuu soka Tanzania akiwa na mabao 17.

Pia timu ya Yanga ambayo ilipasua miamba hadi kufika hatua ya Tano Bora safari hii wameeondolewa na sasa timu tatu ambazo zimebaki kumenyana ni Al Ahly, Mamelod na Wydad.

Yanga ilikuwa ni miongoni mwa timu ambazo zimepata mafanikio makubwa msimu uliopita ikiwemo kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger lakini katika hatua hiyo timu zote ambazo zilifika hatua hiyo zimetolewa.

Tuzo hizo zinatarajia kutolewa Desemba 13 nchini Morocco ambapo mshindi wa jumla atatangazwa siku hiyo.

Tags: