Kocha huyo ana uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania kwani aliwahi kuzifundisha Yanga SC, Polisi Tanzania na Coastal Union
Klabu ya soka ya Namungo FC ya mkoani Lindi, imemtangaza Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Zahera anachukuwa nafasi ya kocha Denis Kitambi ambaye mwanzo wa mwezi huu alitimkia klabu ya Geita Gold.
Kabla ya kujiunga na Namungo, Zahera alianza msimu huu akiwa na kikosi cha Coastal Union ya mkoani Tanga ambapo alifutwa kazi baada ya mechi tano za awali za ligi.
Pia Zahera amewahi kuwa kocha wa timu za Yanga na Polisi Tanzania ambayo alishuka nayo daraja msimu uliopita.
Huyu anakuwa ni kocha wa tatu wa Namungo msimu huu baada ya kuanza na Cedric Kaze kisha Kitambi.
Kocha Zahera anasifika zaidi kwa soka lake la kuwaamini wachezaji vijana ambapo baadaye wanakuja kuwa hazina kwa klabu.
Kikosi cha Namungo kimecheza mechi 14 wakiwa wamekusanya alama 17 na wapo katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.