Kipa huyo tegemeo alicheza mechi yake ya kwanza na Wekundu wa Msimbazi tangu Aprili 7 mwaka huu
Kipa tegemeo wa timu ya Taifa Stars na Simba SC, Aishi Manula, amerejea kuidakia timu hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Dar es Salaam walioibuka na ushindi wa mabao 5-1.
Manula alikuwa nje ya uwanja tangu Aprili 7, mwaka huu ambapo alikuwa akisumbuliwa na nyama za paja alizokwenda kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini.
Alipata majeraha hayo wakati wa mchezo wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Ihefu FC uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliopigwa leo Uwanja wa Mo Arena, Bunju, Manula alianza na kucheza kwa dakika 40 kabla ya kufanyiwa mabadiliko na kuingia Hussein Abel.
Kurejea kwa kipa huyo ni habari njema kwa mashabiki na wanachama wa Simba ambao timu yao inajiandaa na mchezo dhidi ya Al Ahly ya Misri wa michuano ya African Football League (AFL) utakaopigwa Oktoba 20.
Kama ataendelea vizuri na kuwa fiti, Manula anaweza kuanza kucheza katika michuano hiyo.
Katika mchezo huo, mabao ya Simba SC yalifungwa na mshambuliaji mzawa, Shaaban Chilunda mawili na viungo Mcameroon Leandre Willy Essomba Onana, Luis Jose Miquissone kutoka Msumbiji na Mrundi, Saido Ntibanzokiza.