MO Dewji ateua wajumbe 21 Baraza la Ushauri la Simba SC

Ligi Kuu: MO Dewji ateua wajumbe 21 Baraza la Ushauri la Simba SC

Na Zahoro Mlanzi • 16:30 - 29.10.2023

Dewji amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tangu waanze safari ya mabadililko ya klabu yao, wamepiga hatua kubwa.

Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji 'Mo Dewji', ameteua wajumbe 21 wa Bodi ya Baraza la Ushauri wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kupitia mtandao wake wa kijamii wa X, Mo Dewji, amewataja wajumbe hao ni Mwenyekiti, Jaji Thomas Mihayo, Hassan Dalali, Ismail Aden Rage, Evans Aveva, Faroukh Baghoza, Swedi Nkwabi, Azim Dewji, Kassim Dewji, Musleh Al-Ruweh na Mohamed Nassor.

Wengine ni Mulamu Ng’ambi, Octavian Mshiu, Prof. Janabi, Hassan Kipusi, Geofrey Nyange, Gerald Yambi, Moses Kaluwa, Crescentius Magori, Juma Pinto, Mwina Kaduguda na Idd Kajuna.

Pia MO Dewji amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tangu waanze safari ya mabadililko ya klabu yao, wamepiga hatua kubwaa katika nyanja mbali mbali.

"Pamoja na maendeleo ambayo klabu yetu imepiga katika kipindi hiki cha miaka mitano lakini malengo yetu bado hatujayafikia," ameandika MO Dewji katika taarifa hiyo.

Amesema mojawapo ya majukumu yake kama Raisi wa heshima wa Simba ni kuhakikisha uongozi na utawala bora unazidi kuboreshwa kila wakati ili kuzidi kusukuma gurudumu la maendeleo ya klabu hiyo.

Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kuwiana kwa alama na watani zao wa jadi, Yanga, wote wakiwa na alama 18.

Timu hizo zitaumana Jumapili katika mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Tags: