Kocha huyo amewahi kuifundisha Azam kabla ya kuvunjiwa mkataba na nafasi yake kuchukuliwa na Kali Ongala
Kocha wa timu ya KMC, Abdulhamid Moalin, amesema hawezi kurudi Azam FC kwa sasa kwani akili yake ni kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri msimu huu.
KMC kwasasa ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 15 lakini wanaonekana kuwa vizuri hasa kiuchezaji chini ya kocha huyo ambaye aliwahi kufundisha Azam.
Moalin alitoa kauli hiyo mara baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji na kufungwa bao 1-0 wakiwa nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
"Kwasasa akili yangu yote ni hapa KMC, sina taarifa rasmi kama kuna timu inanihitaji ila nimekuwa nikiona na kusikia kwenye mitandao ya kijamii kitu ambacho siwezi kuamini," amesema.
Moalin amewahi kuifundisha Azam kabla ya kuvunjiwa mkataba na nafasi yake kujazwa na Kali Ongala ambaye naye alitimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita.
Kuhusishwa kwa Moalin kurudi Azam kumetokana na timu hiyo kuwa katika kipindi kigumu baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo kitu kilichosababisha nafasi ya Kocha Youssouph Dabo kuwa katika wakati mgumu.