Msuva ajiunga na Al Najmah ya Saudi Arabia

Nyota wa Taifa Stars, Simon Msuva, akishangilia bao alilofunga dhidi ya Zambia

KANDANDA Msuva ajiunga na Al Najmah ya Saudi Arabia

Na Zahoro Juma • 16:24 - 24.01.2024

Nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', kwa sasa yupo na timu hiyo inayocheza michuano ya AFCON inayoendelea nchini Ivory Coast

Winga wa kimataifa wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, amejiunga na Klabu ya Al Najmah FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia.

Msuva ambaye kwasasa yupo na kikosi cha Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya Afcon nchini Ivory Coast, alikuwa ni mchezaji huru mara baada ya kuachana na Klabu ya JS Kabylie ya nchini Algeria mwezi uliopita.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, Moro United na Azam FC, anatarajia kujiunga na timu hiyo mapema mara baada ya kuhitimisha ushiriki wake katika michuano ya Afcon.

Akitoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Msuva, hakutaja muda halisi wa mkataba ambao amesaini.

"Ninayofuraha kuwafahamisha kuwa nimejiunga na timu ya Al-Najmah," amesema.

Katika dirisha la usajili ambalo limefungwa nchini Januari 15, Msuva alihusishwa kujiunga na klabu yake ya zamani ya Yanga lakini uhamisho huo haukuweza kufanikiwa hadi wakati anaondoka kwenda Afcon.

Kwenye maisha yake ya soka ya nje ya nchi, Msuva amewahi kupita katika Klabu za Difaa Hassani El Jadidi na Wydad Casablanca zote za Morocco.

Pia amewahi kucheza katika timu ya Al Qadsiah ya nchini Saudi Arabia kabla ya kurejea tena Afrika na kujiunga na JS Kabylie.

Timu ya Al-Najmah katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza msimu huu, imecheza mechi 18 na imekusanya alama 25 ikiwa katika nafasi ya tisa.

Msuva alitarajia kuwa sehemu ya kikosi cha Stars usiku wa leo ambacho kilitarajia kucheza dhidi ya DR Congo katika mchezo wa mwisho wa kufunga hatua ya makundi.

Kwenye michuano ya Afcon, Msuva, amefunga bao pekee la Stars katika mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Zambia.

Bao hilo limemfanya kuwa mfungaji bora namba mbili wa Tanzania sambamba na Mbwana Samatta wakiwa wana mabao 23 na wanamfukuzia Mrisho Ngassa ambaye ni kinara mwenye mabao 25.

Tags: