Nahodha Mbwana Samatta akiri Morocco ni 'muziki mnene'

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, akimtoka beki wa Morocco,Achraf Hakimi

KANDANDA Nahodha Mbwana Samatta akiri Morocco ni 'muziki mnene'

Na Zahoro Juma • 14:23 - 18.01.2024

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Samatta, amekiri kuzidiwa na Morocco ndio maana wamepoteza mechi ya kwanza ya michuano AFCON.

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta, amekiri kuzidiwa na Morocco ndio maana wamepoteza mechi ya kwanza ya michuano AFCON inayoendelea nchini Ivory Coast.

Taifa Stars ilishuka uwanjani Stade Laurent Pokou katika mchezo wa Kundi F ambapo katika dakika 90 ilijikuta ikifungwa mabao 3-0.

Ushindi huo umeifanya Morocco kuongoza kundi hilo akiwa na alama 3 huku DR Congo na Zambia zikifuata zikiwa na alama 1 kila mojaa ya kutoka sare ya bao 1-1.

Stars ambayo inashiriki kwa mara ya tatu katika fainali hizo, haijawahi kupata ushindi katika mechi saba mfululizo za michuano hiyo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nahodha Samatta ambaye anacheza soka la kulipwa PAOK Thessaloniki FC ya Ugiriki, amesema Morocco walikuwa bora zaidi yao lazima ukweli usemwe.

"Tulijitahidi kucheza kwa nidhamu kwa kufuata maelekezo ya mwalimu lakini ubora wa wapinzani wao ndio uliamua mchezo huo," amesema Samatta ambaye alicheza kwa dakika 69 katika mchezo huo kabla ya kumpisha Feisal Salum 'Fei Toto' kuingia.

Amesema unapocheza na mpinzani kama Morocco na amekutangulia kufunga bao alafu ukiangalia wana wachezaji wanaomiliki mpira kwa muda mrefu inakuwa ngumu kupata mabao.

Amesema kikubwa kwa sasa watajiandaa na mechi zijazo dhidi ya Zambia na Kongo ili kuona jinsi gani wanaweza kupata matokeo mazuri.

"Ni wakati wao benchi la ufundi kuangalia upungufu wa wapinzani wetu waliobaki pamoja na ubora wao ili tupate matokeo mazuri," ameongeza.

Pia amesema wamesikitishwa na matokeo hayo kwani walijiandaa vizuri kukabiliana na Morocco lakini bahati haikuwa upande wao.

Stars mechi inayofuata itashuka uwanjani kuumana na Zambia katika mchezo utakaopigwa Februari 21.

Tags: