Kocha huyo aliwahi kuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ambaye pia aliichezea Yanga SC na Tanzania Prisons
Uongozi wa Klabu ya Namungo ya mkoani Lindi, umesema timu yao kwasasa ipo chini ya Kocha, Shadrack Nsajigwa katika kipindi hiki ambacho wanatafuta kocha wa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Denis Kitambi.
Mapema wiki hii Namungo wametangaza ghafla kuachana na Kitambi ambaye alionekana tayari ameanza kuiweka timu kuwa sawa.
Kitambi alichukuwa timu kutoka mikononi kwa Mrundi, Cedric Kaze ambaye aliiongoza timu hiyo kwenye michezo sita ya kwanza ya Ligi Kuu Bara bila kupata ushindi wowote.
Hata hivyo, baada ya timu kuchukuliwa na Kitambi ndani ya michezo saba, timu imepata ushindi katika michezo minne na kutoa sare mara mbili huku ikikubali kichapo katika mechi moja.
Matokeo hayo yaliwafanya kutoka nafasi ya 14 waliyokuwa nayo mwanzo na kupanda hadi nafasi ya sita wakiwa na alama 17 hadi sasa.
Akizungumza na Pulsesports, Ofisa Habari wa timu hiyo, Omary Kindamba, amesema kwasasa wapo katika mchakato wa kutafuta kocha mpya lakini kwa kipindi hiki timu ipo chini ya aliyekuwa Kocha Msaidizi, Nsajigwa.
"Timu kwasasa ipo chini ya Nsajigwa hadi pale tutakapo tangaza kocha mpya, zoezi la kusaka kocha linaendelea na hivi karibuni tutawajulisha," amesema.
Namungo itashuka uwanjani kesho kwenye Uwanja wa Majaliwa kucheza dhidi ya Hoollwood katika mchezo wa Kombe la FA.