Pacome ashinda bao Bora la Wiki michuano ya CAF

KANDANDA Pacome ashinda bao Bora la Wiki michuano ya CAF

Zahoro Mlanzi • 16:37 - 05.12.2023

Nyota huyo amesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Asec Mimosa ya Ivory Coast

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limechagua bao la kusawazisha alilofunga Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua kwenye mechi dhidi ya Al Ahly kuwa ni bao Bora la Wiki katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mechi za mzunguko wa pili.

CAF wamelichagua bao hilo kuwa bora kati ya mabao yote 15 ambayo yalifungwa katika mzunguko wa pili kwa mechi zote 8 zilizochezwa.

Pacome amefunga bao hilo dakika ya 90 ya mchezo ambalo liliisadia timu yake kuepuka kipigo cha nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi kwenye mchezo wa Kundi D.

Huo ulikuwa ni mchezo wa pili kwa timu zote mbili na matokeo hayo yaliwafanya Yanga kuendelea kuburuza mkia wakiwa wamejikusanyia alama 1 huku Al Ahly wakiwa kileleni na alama zao 4.

Nyota huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea Asec Mimosa, amekuwa na kiwango bora si katika michuano ya kimataifa pekee, kwani hata katika Ligu Kuu Bara anafanya vizuri.

Katika ligi kuu, amefunga mabao manne na asisti mbili katika michezo 9 iliyocheza kwenye ligi hiyo huku yeye akikosekana katika mchezo mmoja dhidi ya JKT Tanzania.

Kiungo huyo pamoja na wenzake, Stephane Aziz KI na Max Nzengeli, wanatarajiwa kushirikiana vizuri katika mchezo wao wa Ijumaa dhidi ya Medeama SC kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga inaburuza mkia ikiwa na alama 1 huku Al Ahly akiongoza akiwa na alama 4 akifuatiwa na Medema na CR Boulzdad zenye alama 3 kila moja.