Robertinho aifungia kazi Prisons

© Kwa Hisani

KANDANDA Robertinho aifungia kazi Prisons

Zahoro Mlanzi • 22:00 - 04.10.2023

Robertinho anakumbuka Juni 26, mwaka jana wakiwa kwenye uwanja huo walikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa maafande hao wa Magereza.

Kocha mkuu wa timu ya Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’, amesema amejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa saa 10 jioni Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Robertinho anakumbuka Juni 26, mwaka jana wakiwa kwenye uwanja huo walikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa maafande hao wa Magereza.

Akizungumza na Pulsesports kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Robertinho amesema anawakumbuka vizuri Prisons sababu waliwapa upinzani mkubwa msimu uliopita lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanawadhibiti.

Amesema kama kawaida wataingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kucheza soka safi na kupata ushindi.

“Tuna siku moja imebaki ya kufanya mazoezi ili kupata timu ya wachezaji 11 watakaoanza kwenye mchezo wa kesho. Tunatarajia kupata upinzani mkubwa.

“Tunawaheshimu Prisons, tunakumbuka msimu uliopita walitupa mechi ngumu lakini tumejipanga, sisi tutaingia uwanjani kwa lengo la kucheza soka safi na kushinda,” amesema Robertinho.

Kwa upande wa Mlinda mlango wa timu hiyo, Hussein Abel, amesema kwa upande wao kila mmoja yupo tayari kuhakikisha anajitoa kwa kila hali kuhakikisha alama tatu zinapatikana.

“Mara zote tunapokutana na Prisons mchezo unakuwa mgumu, lakini tupo tayari kupambana nao lengo likiwa kuhakikisha tunaondoka na alama tatu,” amesema Abel.

Simba itaingia katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya tatu kutokana na alama 9 sawa na Yanga huku Prisons yenyewe ikishika mkia mkiwa alama 1.