Robertinho kubadili kikosi marudiano na Al Ahly

© Kwa Hisani

KANDANDA Robertinho kubadili kikosi marudiano na Al Ahly

Zahoro Mlanzi • 08:00 - 24.10.2023

Mchezo huo utachezwa kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati kwenye Uwanja wa Cairo.

Kocha wa timu ya Simba SC, Roberto Oliviera 'Robertinho', amesema atabadili kikosi chake baadhi ya wachezaji ili kupata matokeo dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Timu hizo zitashuka uwanjani kesho jijini Cairo katika mchezo wa marudiano wa michuano ya AFL ambapo mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kupitia mtandao wao wa kijamii wa X kuelekea mchezo huo, imemnukuu Kocha Robertinho alisema: "Tunafahamu itakuwa mechi ngumu ila tunajua kuna namna tutakavyoingia katika mchezo huu.

"Tutaingia na mpango tofauti na ilivyokuwa katika mechi ya kwanza nyumbani. Nitakuwa na mabadiliko ya wachezaji kwenye baadhi ya maeneo ili kufanikiwa kucheza vizuri na kupata matokeo," amesema Robertinho.

Mchezo huo utachezwa kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati kwenye Uwanja wa Cairo, kila timu ikiwania kutinga nusu fainali ya michuano hiyo mipya barani Afrika.

Katika mchezo wa kesho, Simba ili kusonga mbele inahitaji ushindi pekee au sare ya mabao 3-3 ili kusonga mbele kutokana na wapinzani wao kuwa na faida ya bao la ugenini.

Tayari wawakilishi hao wa Tanzania walishakita kambi tangu Jumamosi kwenye Jiji la Cairo wakiwa na kikosi chao takribani wachezaji wote isipokuwa mlinda lango wao namba moja, Aishi Manula ambaye bado hajawa fiti kwenye mchezo huu na hata hakutumika pia kwenye mechi ya awali.

Simba hawana kumbukumbu nzuri wanapokutana na Al Ahly kwenye uwanja huo, kwani mwaka 2019 walikutana na kisago cha mabao 5-0 kabla ya 2021 kufungwa tena kwa bao 1-0. Michezo yote hiyo ilikuwa ni hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama Simba watavuka kwenye hatua hii basi wana nafasi kubwa ya kukutana na mshindi kati ya Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini au Petro Atletical de Luanda ya Angola ambao nao wanacheza kwenye robo fainali nyingine.

Tags: