Nyota hao wa kimataifa wa Kenya, wamekuwa na msimu mgumu tangu wajiunge na timu hiyo msimu huu
Wachezaji wa kimataifa wa Kenya, Elvis Rupia na Duke Abuya, wameifungia mabao timu yao ya Singida Fountain Gate katika ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya Arusha City, mchezo uliopigwa Uwanja wa Black Rhino jijini Arusha.
Mchezo huo ambao ulikuwa wa upande mmoja ni wa michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambayo bingwa wake hupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Rupia hilo ni bao lake la tatu akifunga tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea Polisi ya Kenya.
Nyota huyo amefanikiwa kufunga mabao mengine katika Kombe la Shirikisho la Afrika bao moja dhidi ya Future ya Misri lakini pia lingine alifunga katika Ligi Kuu Bara.
Rupia amejiunga na Singida FG baada ya kuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu ya Kenya akifunga mabao 27.
Kwa upande wa Abuya, hajaanza vizuri licha ya kupangwa katika baadhi ya mechi kutokana na ushindani uliopo katika timu hiyo, bao hilo huenda likawa mwanzo mzuri kwake.
Bao lingine la Singida FG katika mchezo huo wa ASFC, limefungwa na Kiungo, Yusuph Kagoma na kuiwezesha timu hiyo kusonga katika hatua ya 32 Bora ya michuano hiyo.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Singida FG inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 20 nyuma ya Azam FC yenye alama 28, Yanga alama 24 na Simba alama 22.
Timu hiyo itashuka tena uwanjani Desemba 21 ugenini dhidi ya Geita Gold FC katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.