Simba SC mambo magumu michuano ya CAF

KANDANDA Simba SC mambo magumu michuano ya CAF

Zahoro Mlanzi • 18:35 - 02.12.2023

Timu hiyo imebanwa mbavu kwa kupata alama moja ugenini, ikiwa ni sare ya pili mfululizo katika michuano hiyo

Timu ya Simba SC, imejikuta ikiendelea kuokota alama moja katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka suluhu na Janweng Galaxy ya Botswana.

Mchezo huo ambao ulipigwa Uwanja wa Obed Ichani Chilume, uliopo nje ya Jiji la Gaborone, umehudhuriwa na mashabiki wachache.

Matokeo hayo si rafiki kwa Simba kwani imevuna alama 2 katika mechi mbili huku Galaxy ikiongoza Kundi hilo la B ikiwa na alama 4.

Timu zingine za kundi hilo, Asec Mimosa yenye alama 1 na Wydad Casablanca ambayo haina alama, zilitarajiwa kushuka uwanjani baadaye katika mfululizo wa mechi hizo.

Simba kwa kiasi kikubwa ilitawala mchezo ila ilikosa umakini katika kukwamisha mpira wavuni kutokana na straika wao, Mkongo Jean Baleke kupoteza nafasi zaidi ya mbili za wazi.

Galaxy yenyewe ilionekana kucheza zaidi kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza wakitumia mawinga wao ambao walikuwa na kasi.

Kocha mpya wa Simba, Mualgeria Abdelhak Benchikha, alifanya mabadiliko manne katika mchezo huo akiwatoa Andre Onana, Sadio Kanoute na kuingia Mzamiru Yassin na Clatous Chama, kisha Saido Ntibazonkiza na Kibu na kuingia Luis Miquissone na Mosses Phiri.

Pamoja na hali hiyo, Simba itajutia nafasi iliyopata sekunde ya 55 kupitia kwa Kibu Denis ambaye alikokota mpira na kupiga krosi iliyounganishwa vibaya na Baleke na mpira kutoka nje.

Lakini pia, Galaxy ilijibu shambulizi hilo dakika ya 9 baada ya Daniel Msendamn, kuwapiga chenga wachezaji zaidi ya watatu wa Simba na kupiga shuti lilookolewa kwa mguu na Kipa, Ayoub Lakred.

Simba ilipata nafasi nyingine dakika ya 24 ambapo Baleke alipiga shuti ndani ya eneo la hatari na kudakwa na Kipa, Phoko Gesione akiunganisha krosi ya Shomari Kapombe.

Katika dakika 4 za nyongeza, Chama alipiga shuti lililogonga mwamba na mpira kumkuta Baleke ambaye alipiga shuti lililopaa juu ya goli.

Michuano hiyo itaendelea tena Desemba 8 ambapo Simba itakuwa ugenini kuumana na Wydad Casablanca.

Tags: