Simba SC yaachana na Robertinho

Breaking News Simba SC yaachana na Robertinho

Zahoro Mlanzi • 13:48 - 07.11.2023

Simba imefikia hatua hiyo ikiwa zimepita siku mbili tangu wafungwe mabao 5-1 na watani zao wa jadi, Yanga katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara

KLABU ya Simba, imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba wa Kocha wao, Roberto Oliviera 'Robertinho'.

Lakini pia klabu hiyo, imefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wa Kocha wao wa viungo, Carneille Hategekimana.

Simba imefikia hatua hiyo ikiwa zimepita siku mbili tangu wafungwe mabao 5-1 na watani zao wa jadi, Yanga katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, Robertinho ameachana na timu hiyo akiwa na rekodi nzuri katika Ligi Kuu tangu atue mwaka jana, amepoteza mechi moja pekee dhidi ya Yanga huku akiiongoza timu hiyo kushinda mechi 29 za ligi hiyo.

Amewahi kupoteza katika michuano ya kimataifa msimu uliopita dhidi ya Raja Casablanca na Horoya AC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo katika mtandao wao wa X na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Iman Kajula, imeeleza:" Uongozi wa Klabu ya Simba unawashukuru makocha hawa kwa mchango wao ndani ya klabu yetu na inawatakia kila la heri katika majukumu yao mapya.

Taarifa hiyo imeeleza katika kipindi hiki cha mpito kikosi chao kitakuwa chini ya Kocha, Daniel Cadena akisaidiwa na Seleman Matola.

Imeongeza mchakato wa kutafuta mkaocha wapya umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde.

Kumekuwa na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zikimtaja aliyewahi kuwa kocha wao, Sven Vandenbroeck kuja kurithi mikoba yake.

Vandenbroeck mara ya mwisho alikuwa akiinoa CR Belouizdad ya Algeria.

Tags: