Simba SC yafunga mwaka kwa sare 2-2 na KMC

LIGI KUU Simba SC yafunga mwaka kwa sare 2-2 na KMC

Zahoro Mlanzi • 20:00 - 23.12.2023

Matokeo hayo yameifanya Simba SC kubali katika nafasi ya tatu ikiwa na alama 23

Klabu ya Simba, imefunga mwaka kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Sare hiyo imewafanya Simba kuumaliza mwaka 2023 wakiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kuvuna alama 23 kwenye michezo 10 walioshuka uwanjani.

Katika mchezo huo, KMC ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la uongozi dakika ya 30 ya mchezo likifungwa na Waziri Juniir aliyetumia mpira wa adhabu wa haraka uliopigwa na Awesu Awesu.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko ingawa kama KMC wangekuwa makini wangeweza kupata bao la ziada kutokana na nafasi walizotengeneza.

Kipindi cha pili, kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko ambapo aliwatoa Willy Onana na John Bocco na nafasi zao kuchukuliwa na Muzamiru Yasin na Jean Baleke.

Mabadiliko hayo, yalizaa matunda kwa Simba kwani dakika ya 57 walipata mkwaju wa penalti baada ya mlinzi wa KMC, Ismail Gambo kuunawa mpira ndani ya boksi.

Penalti hiyo ilifungwa kwa ustadi na Saido Ntibanzokiza na kufanya mambo kuwa 1-1.

Bao la pili la Simba, lilifungwa dakika moja baadaye kupitia kwa Jean Baleke ambaye aliitumia vyema pasi ya Shomari Kapombe.

Baada ya mabao hayo, Simba ilionekana kuutawala zaidi mchezo huku wakitengeneza nafasi nyingi ambazo hawakuzitumia.

Zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika, Junior alirejea kambani baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na Kipa, Ayoub Lakred kutokana na shuti la nje ya eneo la hatari lililopigwa na Tepsi Evans.

KMC sasa wanasalia nafasi ya nne wakiwa na alama 21.

Katika mchezo huo, kiungo fundi wa Simba, Clotus Chama hakucheza kama ilivyoelezwa awali kwamba amesimamishwa na uongozi kutokana na masuala ya kinidhamu.

Tags: