Ni baada ya kuifunga Geita Gold bao 1-0 na kujikusanyia alama 33 huku Azam ikiwa na alama 32
Bao pekee lililofungwa na kiungo wa kimataifa wa Senegal, Babacar Sarr, limeiwezesha timu yake ya Simba SC kuibuka na ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Geita Gold katika mfulilizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ushindi huo, umeifanya Simba kufikisha alama 33 na kupanda hadi nafasi ya pili nyuma ya Yanga SC iliyo kileleni ikiwa na alama 40 ila ipo mbele kwa mchezo mmoja zaidi ya wapinzani wake hao.
Azam ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikiongoza ligi hiyo kabla ya mechi za viporo kuchezwa, imeshuka hadi nafasi ya tatu ikiwa na alama 32.
Sarr ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo akiwa mchezaji huru, aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Sadio Kanoute na kufunga bao hilo pekee dakika ya 82 akiitendea haki pasi ya kichwa iliyopigwa na Kibu Denis.
Kabla ya kufungwa kwa bao hilo, Simba ilikuwa imeliandama kwa muda mrefu lango la Geita Gold lakini tatizo likawa kumalizia mipira ya mwisho kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Geita.
Mashabiki wa soka nchini, wakiwa wanaamini timu hizo zitagawana alama kwani katika dakika 15 za mwisho Geita ilishaamua kukaa nyuma ya mpira huku ikifanya mashambulizi ya kushtukiza.
Hata hivyo, Simba itajilaumu yenyewe kwa kushindwa kufunga mabao ya mapema kupitia kwa Clatous Chama, Kanoute na Par Omar Jobe kwani mashuti yao yalitoka nje na mengine kuzuiwa na mabeki wakiwa katika nafasi ya kufunga.
Licha ya Geita kukaa nyuma ya mpira muda mwingi, ilipata nafasi mbili za wazi katika dakika tano za nyongeza kupitia kwa Tariq Seif ambaye alipiga kichwa kilichotoka sentimeta chache goli pamoja na Nassor Saadun akiwa ndani ya eneo la hatari kupiga shuti lililopaa juu ya goli.
Simba itashuka tena uwanjani Februari 15 kuumana na JKT Tanzania katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo huku Geita yenyewe itacheza na Ihefu Februari 19.