Timu hiyo tayari imeshakata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo na bado ina mchezo mmoja dhidi ya APR ya Rwanda
Timu ya Simba SC, imedhamiria kumaliza mechi zake zote za hatua ya makundi ya michuano ya Mapinduzi Cup kwa ushindi.
Hayo amesema Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Seleman Matola wakati akieleza maandalizi kuelekea mchezo wao wa kesho dhidi ya APR kutoka Rwanda.
Simba ambao ipo Kundi B hadi sasa wana alama 6 baada ya kushinda mechi mbili za awali dhidi ya JKU na Singida FG na tayari wameshatinga hatua ya robo fainali.
Hata hivyo licha ya kutinga hatua hiyo lakini Benchi la Ufundi la Simba, limesema bado linaichukuliwa kwa umuhimu sawa michezo yote inayokuja mbele yao ikiwemo huo wa APR.
"Kama mnavyoona sisi katika michuano hii tupo na malengo makubwa na tunataka kufanya vizuri katika michezo yote," amesema Matola.
Aidha Matola hakusita kuwapa sifa kikosi cha APR ambao ni mabingwa wa Rwanda.
Matola amesema timu hiyo ina kikosi chenye wachezaji bora na hivyo mchezo huo hautakuwa rahisi kwani kila timu itataka kutamba.
Mbali na mchezo huo ambao utapigwa saa 2: 15 usiku, kutapigwa mchezo mwingine saa 10 jioni kati ya Jamhuri FC dhidi ya Jamusi FC ya Sudani Kusini.