Simba, Yanga zatamba kutinga robo fainali Afrika

Simba, Yanga zatamba kutinga robo fainali Afrika

Zahoro Mlanzi • 21:15 - 06.10.2023

Droo hiyo imefanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini, ambapo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, imepangwa Kundi D.

Saa chache baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kupanga ratiba ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu za Simba SC na Yanga SC kujua wapinzani wao, timu hizo zimetamba kufanya vizuri.

Droo hiyo imefanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini, ambapo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, timu ya Yanga, imepangwa Kundi D lenye timu za mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri, CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Simba yenyewe ipo Kundi B lenye timu za Wydad Athletic ya Morocco, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Wakati Kundi A kuna Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Pyramids ya Misri, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nouadhibou ya Mauritania.

Kundi C linazikutanisha Esperance, Etoile Du Sahel za Tunisia, Petro Atlético ya Angola na Al Hilal ya Sudan.

Baada ya droo hiyo, Meneja Mawasiliano na Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, amesema ni kipimo sahihi kwao kupangwa na timu hizo ambapo watatakiwa kuonesha ubora wao katika kuelekea kutimiza mpango wao wa kuijenga timu yao upya.

"Ni Kundi zuri kwetu ambalo litatoa kipimo halisi ya ubora wa timu tuliyonayo, malengo yetu ni kuhakikisha tunafuzu kucheza robo fainali msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika," amesema Kamwe.

Kwa upande wa Meneja Mawasiliano na Habari wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema malengo makubwa ni kutinga hatua ya robo fainali.

“Baada ya kuona wapinzani wetu na timu ambazo tutacheza nao hatuna mashaka ni maandalizi kwa ajili ya mechi hizo ambazo zitafanyika hivi karibuni.

Tumeliona kundi letu namna lilivyo na tuna wachezaji bora pamoja na benchi la ufundi lenye mbinu hivyo tukutane robo fainali,” ametamba Ally.

Tags: