Ametwaa tuzo hiyo baada ya kufunga mabao matano katika michuano hiyo
Uongozi wa Klabu ya Singida FG, unajivunia mafanikio ya mshambuliaji wao, Mkenya Elvis Rupia kwa kuibuka Mfungaji Bora kwenye michuano ya Mapinduzi Cup iliyohitimishwa mwishoni mwa wiki visiwani Zanzibar.
Rupia ameshinda tuzo hiyo kwa kufunga mabao matano na kumzidi kete Allasane Diao wa Azam ambaye alimaliza na mabao manne.
Tuzo hiyo sasa inakwenda Singida FG kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuichukuwa tena mwaka jana kupitia kwa mshambuliaji wao Francy Kazadi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Masanza, amesema licha ya kuwa wamekosa kombe lakini zawadi hiyo pia imewapa moyo katika mashindano hayo.
Amesema walipanga kufanya vizuri zaidi ya mwaka jana lakini bahati haikuwa yao mara baada ya kuondoshwa na Simba katika hatua ya nusu fainali.
"Tulipanga kufanya vizuri zaidi lakini tumeishia nusu fainali, imetusikitisha lakini walau zawadi hii ya ufungaji bora imetupa faraja," amesema.
Msimu uliopita wa michuano hiyo, Singida FG walifika hadi hatua ya fainali ambapo walishuhudia wakipoteza mchezo mbele ya Mlandege kwa kufungwa mabao 2-0.