Licha ya kuwa jina la kocha huyo sio maarufu masikioni mwa wadau wengi wa soka lakini ana uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania
Klabu ya Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya, imemtangaza Hamad Hamis Ally kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho akichukuwa nafasi ya Fred Felix 'Minziro' aliyetimuliwa hivi karibuni.
Kocha huyo ameingia mkataba wa miaka miwili na anatarajia kuanza kazi yake kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji itakayopigwa Novemba 29.
Licha ya kuwa jina la kocha huyo sio maarufu masikioni mwa wadau wengi wa soka lakini ana uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania akiwa amepita katika klabu kadhaa kama kocha msaidizi.
Ally alikuwa ni kocha msaidizi wa kikosi cha Mbao FC ya Mwanza wakati huo wakifundishwa na Kocha, Etienne Ndayiragije.
Baada ya kutoka hapo alijiunga tena na Ndayiragije katika kikosi cha KMC ambapo aliendelea kuwa kocha msaidizi kwa walimu wote waliopita ndani ya timu hiyo hadi alipotangazwa kuitumikia Prisons.
Anakubali jukumu la kuifundisha Prisons ambayo haijaanza vizuri msimu huu ikiwa inashika nafasi ya 15 wakiwa na alama 7 baada ya kushuka dimbani mara 9.
Ally anakuwa kocha wa saba kupata ajira mpya tangu kuanza kwa msimu huu wa 2023/24 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na tayari makocha saba kuwa wamefukuzwa kazi.