Uingereza kuinua Soka la Vijana, Wanawake Simba SC, Yanga SC

Ligi Kuu Uingereza kuinua Soka la Vijana, Wanawake Simba SC, Yanga SC

Na Zahoro Mlanzi • 21:30 - 31.10.2023

Taifa hilo kubwa kisoka ulimwenguni limependa mipango ya klabu hizo jinsi zinavyojipambanua kwenye soka la wanawake na vijana

Serikali ya Uingereza , imeahidi kushirikiana na Klabu za soka za Simba na Yanga katika sekta ya maendeleo ya soka hasa ya vijana na wanawake.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar ambaye ametembelea klabu hizo kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam na kukutana na viongozi wa juu klabu hizo na kufanya nao mazungumzo.

Akiwa ndani Klabu ya Simba ambapo ndipo alipoanzia ziara yake, Balozi Concar, amesema amevutiwa na kiwango cha Simba na hasa ushiriki wao kwenye michuano ya AFL ambapo walitolewa na Al Ahly ya Misri.

"Nimependa mipango ya klabu hii na hasa jinsi inavyojipambanua kwenye soka la wanawake na vijana," amesema.

"Ushiriki wenu katika michuano ya AFL ulikuwa ni ujumbe tosha kuonesha ukubwa wa klabu hii ya kihistoria, hapa Tanzania na Afrika," amemalizia.

Kwa upande wa uongozi wa Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah 'Try Again', amesema wao kama klabu wanashukuru kwa ujio wa Balozi huyo na hasa kwa kuthamini klabu yao.

Amesema mipango ambayo wameipanga na Balozi Concar ni ya kimaendeleo na kwamba haitakuwa na msaada kwa Simba tu bali taifa zima na klabu nyingine pia zitanufaika.

Mbali na Mwenyekiti wa Bodi, baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo ambao walikuwepo kwenye tukio hilo ni Hussein Kitta na Asha Baraka ambao waliongozana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Iman Kajula.

Katika ziara yake hiyo, Balozi Concar, pia ametembelea Uwanja wa Bunju Arena ambapo timu ya wakubwa ya wanaume ya Simba inafanya mazoezi ikijiandaa na mchezo wake wa 'derby' dhidi ya Yanga Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa.

Baada ya kumaliza ziara yake ndani ya Simba, Balozi Concar amefunga safari hadi kwenye ofisi za Yanga ambapo napo alipokelewa na uongozi wa juu ukiongozwa na Rais, Injinia Hersi Said, Makamu wake, Arafat Hajji na watendaji wengine.

Katika mazungumzo yake na viongozi hao kama ilivyokuwa kwa Simba, Balozi Concar amewapongeza Yanga kwa namna wanavyoiongoza timu yao kiweledi na pia kwa mafanikio waliyopata kwa mashindano mbalimbali ya ndani na nje.

Aidha Balozi huyo ametembelea wachezaji wa Yanga ambao wanajifua kwenye kambi ya mazoezi Aviv Town, Kigamboni wakijiandaa na mchezo wa Jumapili dhidi ya watani zao wa jadi, Simba.

Tags: