Timu hiyo ili kujiweka katika nafasi ya kutinga robo fainali haina budi kuibuka na ushindi
Timu ya Yanga SC, leo saa 1 usiku itashuka uwanjani kuumana na CR Belouizdad katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ukiwa ni mchezo wa hukumu.
Hukumu hiyo inatokana na timu hizo kuwa zinashuka uwanjani kila moja ikiwa na alama tano zikishika nafasi ya pili na ya tatu katika Kundi D huku Al Ahly ambayo ndio kinara kwa kuwa na alama tisa na Medeama ikishika mkia kwa alama nne.
Ahly imefikisha alama hizo baada ya usiku wa kuamkia leo kuitandika Medeama FC ya Ghana kwa bao 1-0, hivyo imeshakata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo.
Yanga, ili ijihakikishie kuungana na Al Ahly katika kucheza robo, haina budi kuifunga Belouizdad katika mchezo wa leo ambapo itakuwa imefikisha alama nane, hivyo mechi ya mwisho dhidi ya Ahly atahitaji kupata alama moja ili afuzu.
Kuelekea mchezo huo, Uongozi wa Yanga, uliiipa jina maalum 'Pacome Day' na baadhi ya nyota wa timu hiyo wameshaanza kuiga mtindo wa nywele unaotumiwa na kiungo, Pacome Zouzoua ambaye nywele zake amepaka rangi nyeupe ' bleach'.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, akizungumzia maandalizi kwa ujumla wake, amesema ni mchezo mgumu lakini atahakikisha wanapambana kupata matokeo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali.
"Hakuna matokeo tunayoyahitaji zaidi ya ushindi, tutapambana kuhakikisha hilo linatokea ili kujiweka katika nafasi nzuri, CR Belouizdad ni timu nzuri barani Afrika hivyo pia tutacheza kwa tafadhali," amesema Gamondi.
Mchezo huo utakaoanza saa 1 usiku kwa saa Afrika Mashariki na Kati, utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.