Timu hiyo inashika mkia kutoka Kundi B baada ya kuvuna alama 1 katika mechi mbili ilizocheza huku Al Ahly akiongoza akiwa na alama 4
Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Al Ahly, Klabu ya soka ya Yanga, sasa wamehamishia nguvu zao kwenye mechi yao ya ugenini dhidi ya Medeama FC ya kutoka nchini Ghana.
Mechi hiyo inatarajia kupigwa Desemba 8 na wawili hao watarudiana tena Desemba 20 ikiwa ni katika mechi mbili zilizofuatana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Akizungumza baada ya mchezo wa Al Ahly uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kutoka sare ya bao 1-1, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema hesabu zao bado hazijaharibika na kwamba wana jambo lao dhidi ya Medeama.
Amesema walipanga kushinda mechi dhidi ya Al Ahly lakini bahati haikuwa kwa upande wao na mchezo huo umekwisha sasa wanaanza maandalizi ya mechi iyayo.
"Tulipanga na tulijiandaa kupata alama tatu leo (juzi) lakini mechi imechezwa imeonekana, jitihada zetu hazikuzaa matunda, hata hivyo bado tupo kwenye ushindani kuna alama 12 zimebaki kwa ajili ya kuzigombea," amesema.
Amesema kutokana na umuhimu wa mchezo huo timu itaingia kambini haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo ambao watalazimika kusafiri kwenda nchini Ghana.
Medeama ambao ni mabingwa wa Ghana wao wana alama tatu hadi sasa baada ya kupata ushindi wa nyumbani kwenye mechi yao ya Ijumaa dhidi ya CR Belouizdad ambao nao wana alama tatu ambazo walizipata kwa kuwafunga Yanga 3-0 kwenye mchezo wa kwanza.
Yanga kwa upande wao bado wanasaka ushindi wao wa kwanza kwenye michuano hiyo hatua ya makundi.
Kumbuka kwa Yanga walifika hatua kama hiyo mara ya mwisho mwaka 1998 na walishindwa kusonga mbele baada ya kuambulia alama 1 katika mechi 6 walizocheza huku wakiwa hawajapata ushindi wowote.