Mchezo wa mwisho wa Kundi D wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ndio utakaotoa kinara wa kundi hilo
Uongozi wa Klabu ya Yanga SC, umesema timu yao ipo tayari kucheza na mpinzani yeyote katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imefuzu kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu yao baada ya kuifunga CR Belouizdad kwa mabao 4-0 kwenye mechi iliyochezwa Jumamosi Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo uliwavusha Yanga moja kwa moja kwenye hatua hiyo ingawa imebakiwa na mchezo mmoja ambao watamalizia dhidi ya Al Ahly Ijumaa kuanzia saa 1 usiku.
Kuelekea mchezo huo dhidi ya Al Ahly, kikosi cha Yanga kimeondoka jioni ya leo kwenda nchini Misri na kinatarajiwa kufika kesho alfajiri na kitaanza maandalizi kwa ajili ya mchezo huo.
Yanga imetua Misri ikiwa na msafara wa watu zaidi ya 60 wakiwemo wachezaji 24, wataalamu wa benchi la ufundi 13 na maofisa mbalimbali wa timu hiyo ambao ni mabingwa mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema timu yao inafanya maandalizi kwa ajili ya kushinda mchezo huo na ndio maana wamesafiri na kikosi chote kwa wachezaji ambao ni wazima.
Amesema wanalenga kupata ushindi kwenye mchezo huo ili waweze kuongoza kundi lakini hata ikitokea wakisalia katika nafasi ya pili hawana shaka na mpinzani yoyote watakayekutana naye katika hatua ya robo fainali.
"Tunajiandaa kwa ajili ya ushindi katika mechi yetu ya mwisho lengo ikiwa ni kumaliza vinara wa Kundi D lakini hata kama tutamaliza katika nafasi ya pili bado hatuna shida ya kukutana na mpinzani yeyote atayepangwa kucheza na sisi," amesema.
Yanga kama watamaliza katika nafasi ya pili atalazimika kupangwa na timu zilizomaliza nafasi ya kwanza kutoka katika makundi ya A, B na C.
Hadi sasa timu pekee ambayo imejihakikishia kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi lake ni Asec Mimosa tu kutoka katika Kundi D ambapo pia wapo watani wa jadi wa Yanga, timu ya Simba.
Timu nyingine ambazo zinaweza kumaliza katika nafasi ya kwanza katika makundi yao kama wataepuka vipigo katika mechi zao za mwisho ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Petro Athletico ya Angola.