Yanga SC yajivunia kufanya usajili bora mwaka huu

©Yanga (Twitter).

KANDANDA Yanga SC yajivunia kufanya usajili bora mwaka huu

Na Zahoro Mlanzi • 18:34 - 29.12.2023

Tambo hizo zinatokana na mwenendo mzuri waliokuwa nao katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki

Uongozi wa timu ya Yanga SC, umeweka wazi una kila sababu za kujivunia uwepo wa wachezaji wao wote wanaofanya kazi kwa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kiungo, Stephane Aziz Ki.

Aziz Ki ndiye mchezaji namba moja kwenye utupiaji mabao ndani ya Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 10 kibindoni sawa na namba ya jezi yake pendwa mgongoni akiwa uwanjani kutimiza majukumu yake.

Bao la 10 alifunga katika mchezo wa mwisho ndani ya mwaka huu dhidi ya Tabora United, mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na ubao ulisoma Tabora United 0-1 Yanga.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, wana wachezaji wengi wanaofanya vizuri jambo ambalo linafanya wajivunie uwepo wao.

“Kuna wachezaji wanaofanya kazi kubwa uwanjani wote kwa ushirikiano hilo ni muhimu. Hata anayeongoza kwa kufunga sio mshambuliaji kama ambavyo wanasema lakini anatoka Yanga hilo lipo wazi," amesema Kwamwe. 

“Ikiwa ipo hivi basi nao wanaotusema watuambie mshambuliaji wao yuko wapi na kipi ambacho kinafanyika. Hakuna namna ni lazima tuwapongeze wachezaji wetu wanafanya kazi kubwa kutimiza majukumu yao.” 

Timu hiyo inatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi Cup ambayo imeanza jana.

Yanga itacheza mchezo wao wa kwanza Jumapili dhidi ya Jamhuri FC, mchezo utakaopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani humo.