Yanga yapigwa 2-1 na Ihefu FC Ligi Kuu

© Kwa Hisani

KANDANDA Yanga yapigwa 2-1 na Ihefu FC Ligi Kuu

Zahoro Mlanzi • 21:00 - 04.10.2023

Matokeo hayo ni kama yaliyotokea Novemba 29, mwaka jana kwenye uwanja huo huo ambapo 'unbeaten' ya Yanga iliishia hapo kwa kufungwa idadi kama hiyo ya mabao.

Timu ya timu ya Yanga SC, imejikuta ikiduwazwa na Ihefu FC kwa mara nyingine kwenye Uwanja wa Highland Estate mjini Mbarali, Mbeya kwa mabao 2-1 katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Matokeo hayo ni kama yaliyotokea Novemba 29, mwaka jana kwenye uwanja huo huo ambapo 'unbeaten' ya Yanga iliishia hapo kwa kufungwa idadi kama hiyo ya mabao.

Katika mchezo huo ulioisha muda si mrefu, Yanga pia iliingia uwanjani ikiwa haijaruhusu bao tangu msimu huu kuanza zaidi ya kuruhusu kwa mkwaju wa penalti katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASAS ya Djibout ambapo walishinda 5-1.

Matokeo hayo, yameifanya Yanga kubaki katika nafasi ya pili ikiwa na alama 9 sawa na Simba SC ambayo kesho itashuka uwanjani kuumana na Prisons huku Ihefu ikipanda hadi nafasi ya saba ikiwa na alama 6.

Mabao ya Ihefu katika mchezo huo, yamefungwa na Leny Kissu na Charles Ilanfya huku bao pekee la Yanga likifungwa na Pacome Zouzoua ikiwa ni bao lake la pili katika michuano hiyo.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, imefanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake cha kwanza kwa kuwaanzisha wachezaji wazawa saba tofauti na ilivyozoeleka kitu ambacho kiliwarahisishia kazi Ihefu katika dakika 45 za kwanza licha ya kwenda sare ya bao 1-1.

Yanga ndio imekuwa ya kwanza kufunga bao dakika ya 3 kupitia kwa Zouzoua ambaye aliunganisha vizuri mpira uliopigwa na Clement Mzize aliyemzidi kasi beki mkongwe, Juma Nyosso na kuuwahi mpira uliorushwa na Kibwana Shomari.

Pamoja na uwanja kutoonekana si rafiki kwa Yanga, Ihefu wao hawakuwa na shida kwani wametumia zaidi mipira mirefu wakimpigia Ilanfya ambaye aliwapa wakati mgumu mabeki wa Yanga.

Kisu amewainua mashabiki wa Ihefu dakika ya 40 baada ya kufunga bao kwa kichwa akikutana na mpira uliotemwa na Kipa, Djigui Diarra aliyepangua mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Never Tigere.

Pia kipindi cha kwanza, Tigere nusura angefunga bao baada ya shuti alilopiga nje ya eneo la hatari kupanguliwa na Diarra na kuwa kona tasa lakini Mzize naye alikosa bao kwa kichwa akipiga nje akiunganisha mpira wa kona wa Zouzoua.

Dakika ya 66, Ilanfya alifunga bao la ushindi kwa shuti ndani ya eneo la hatari baada ya kukutana na mpira uliopigwa na Joseph Mahundi na kujaa wavuni huku Diarra akiruka bila mafanikio.

Ligi hiyo itaendelea kesho saa 10 jioni ambapo Prisons itaumana na Simba SC katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Msimu uliopita Simba ililala kwa bao 1-0 uwanjani hapo.